Miaka 30 Jela kwa Kusafirisha Dawa za Kulevya

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu Mkazi wa Tabata, Lina Muro kwenda jela miaka 30 baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya, pamoja na hukumu hiyo simu nne alizokutwa nazo pia zimetaifishwa.

Hukumu hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Agustina Mbando baada kupitia ushahidi wa Mashahidi saba wa upande wa mashitaka ikidaiwa kuwa Januari 26, 2018 huko Tabata Bima NSSF Mshitakiwa huyo alikuwa akisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa gramu 43.95.

Hakimu Mbando alisema, baada ya kupitia ushahidi wa Mashahidi wote 7 pamoja na vielelezo, Mahakama hiyo imejiridhisha pasipo shaka hivyo inamtia hatiani, kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa utetezi Nehemia Nkoko aliiomba Mahakama kumpunguzia adhabu kwa kuwa Mtuhumiwa bado ni Kijana na nguvu kazi ya Taifa na pia ana Mtoto mdogo anaemtegemea.