WATOTO NI WAO LAKINI KWENDA SHULE NI LAZIMA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ni jukumu ya kila mzazi kuhakikisha anampeleka shule mtoto kwa kuwa Serikali imeweka mazingira bora na wezeshi katika Sekta ya Elimu
“Tulishasema, mtoto wa Kitanzania kwenda shule ni lazima. Watoto ni wao, lakini kwenda shule ni lazima. Ndiyo maana Serikali ilifuta ada katika shule zote.”
Alitoa kauli hiyo jana mchana (Jumanne, Desemba 28, 2021) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Lindi waliofika kumpokea kwenye uwanja wa ndege wa Nachingwea, mkoani humo.
Waziri Mkuu alisema ujenzi wa madarasa unaoendelea kote nchini hivi sasa, unalenga kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anakwenda shule iwe ni ya msingi au ni ya sekondari. “Tunataka tuondoe kabisa tabia ya kukuta watoto wetu wakifanya biashara kwenye stendi za mabasi au nyumba za starehe.”
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao wawahimize wananchi watunze akiba ya chakula walichonacho kwa sababu mkoa wa Lindi ni miongoni mwa mikoa ambayo bado haijaanza kupata mvua za vuli.
“Lindi ni miongoni mwa mikoa ambayo haijapata mvua hadi sasa. Lazima tujipange, tuangalie kwani yako mazao ya kibiashara na yako pia mazao ya chakula ambayo yanatumika kibiashara. Tutunze akiba tuliyonayo, tusitumie akiba hii kutengeneza pombe au kufanyia sherehe,” alisema na kuwasisitiza viongozi hao wakatoe elimu kwa wananchi.
You must be logged in to post a comment.