RAIS wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi “Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Badilikeni”

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza haja kwa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kubadilika kwani hariziki na jinsi sekta ya Utalii inavyoendeshwa hasa ikizingatiwa kwamba uchumi wa Zanzibar unategemea sekta hiyo.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na uongozi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale pamoja na baadhi ya Watendaji wa Wizara hiyo katika mkutano maalum wa kuwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa maagizo waliyopewa Mawaziri pamoja na Makatibu Wakuu wakati wa hafla ya kuapishwa.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa uchumi wa Zanzibar kwa kiasi kikubwa unategemea sekta ya utalii lakini bado hajarizika na utalii unavyoendeshwa na kuna haja ya mambo mengi katika sekta hiyo kuyafanywa kinyume na ilivyo hivi sasa.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba miongoni mwa juhudi ambazo zinahitajika kwa kiasi kikubwa ni kuitangaza zaidi sekta ya utalii ili kuona maendeleo yanapatikana kama ilivyokusudiwa.

Aliongeza kuwa dhima ya mikutano hiyo anayoiendesha Ikulu ni kurekebisha utendaji hivyo kuna kila sababu kwa Wizara hiyo kubadilika ili kuhakikisha sekta ya utalii inafikia yale malengo yaliyokusudiwa katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja ya kuwa na chombo maalum cha Utalii kikiwa na azma ya kuimarisha uchumi wa Zanzibar.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi akaeleza kutokuwa na ulazima wa kuwepo kwa programu nyingi katika Wizara hiyo na badala yake zikapunguzwa kwa lengo kufikia mafanikio yaliyokusudiwa.

Akieleza kuhusu makumbusho, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja ya kuyafanyia utaratibu maalum makubusho ya Zanzibar ambayo utapelekea makumbusho hayo kufanya kazi badala ya kuwa kama yalivyo hivi sasa kwani moja ya vitu vinavyochangia mapato ya utalii ni makumbusho.

Pia, alieleza umuhimu wakukusanywa fedha kwa njia ya elektroniki hatua ambayo itaondosha kupotea ama kuvuja kwa mapato katika sekta ya utalii.
Kwa upande wa nyumba za Mji Mkongwe wa Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja kwa Wizara hiyo kutafuta wawekezaji wa kuekeza kwa baadhi ya nyumba walizozitenga sambamba na kuimarisha miundombinu ya Mji huo ili uwe Mji Mkongwe wa kitalii.