Makamu wa Rais |Rais Magufuli anawasalimia sana

Samia Suluhu Hassan makamu rais wa Tanzania
“Katika wakati muhimu wa Watanzania kushikamana ni wakati huu, wakati wa kujenga umoja ni huu, sio wakati wa kusikiliza maneno ya kutoka nje yakatuparaganisha, tuchape kazi, tujenge umoja ili Tanzania iwe Taifa imara”-Mama Samia Suluhu, Makamu wa Rais wa Tanzania akiwa ziarani Tanga
“Niwahakikishie Wananchi, Tanzania tuko salama, chapeni kazi ili kuleta maendeleo, uimara wa Taifa letu unaleta maneno mengi, msibabaishwe na maneno ya Watu walioko nje”

Makamu wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tanga.

Amesema kuwa rais Magufuli anawasalimia sana Watanzania na anawasihi waendelee kuchapa kazi.

‘’Mheshimiwa rais anawasalimia na anawashukuru sana sana, kwa kazi nzuri mlioifanya mwaka jana mwezi wa kumi ya kurudisha serikali ya chama cha mapinduzi madarakani, anasema tuko salama, tuchape kazi, tujenge upendo na mshikamano.’’ Anasema Samia Suluhu.

Mama Samia amewataka pia watanzania kuacha kusikiliza maneno ya watu wa nje na kuwa na umoja katika wakati huu. 

‘’Nataka niwaambie kwamba katika wakati muhimu wa watanzania kushikamana ni wakati huu, kujenga umoja ni wakati huu, si wakati wa kusikiliza maneno yanayotoka nje nasi yakatuparaganya vichwa, uimara wa taifa letu unaleta maneno mengi.’’ Anasema Makamu wa rais Samia suluhu. 

Kauli hii ya makamu wa rais inakuja wakati kukiwa na uvumi katika mitandao ya kijamii kuhusu kutokuonekana kwa rais John Magufuli. 

Hadi sasa watu wanne wamekamatwa kwa tuhuma za kusambaza uvumi kwenye mitandao ya kijamii kuwa rais Magufuli anaumwa. 

Mara ya mwisho kwa rais Magufuli kuonekanaka hadharani ilikuwa Jumamosi ya Februari 27 hali amabayo imezua fununu na maswali juu ya alipo na hali yake kiafya. 

Siku ya Ijumaa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alivunja ukimya na kueleza kuwa rais Magufuli anaendelea na shughuli zake kama kawaida na si lazima aonekane kila siku