Mahakama Kuu kanda ya Tabora imemuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa Ntuluwambula Ukenyenge almaarufu Abasi Charles Mkazi wa Kata ya Usinge wilayani Kaliua baada ya kutiwa hatiani kwa kumuua ndugu yake Masayu Salum na kisha kumfukia kwenye shimo.

Katika hati ya maelezo ya onyo ya mshitakiwa yaliyowasilishwa mahakamani hapo na wakili upande wa Jamhuri, Gladness Senya iliyotolewa na shahidi mmoja kati ya mashahidi kumi, mshtakiwa alibainisha kuwa alimuua ndugu yake huyo Julai 23, 2014 kwa maelekezo ya baba yake mzazi ikiwa ni imani za kishirikina ‘NDAGU’ au ‘KAFARA’ ya kutaka utajiri wapate mifugo mingi zaidi ndani ya familia yao.
Maelezo hayo pia yalibainisha kwamba mshitakiwa alikiri baada tu ya kufanya mauaji hayo katika Kijiji cha Matanda huko Ussoke Mlimani wilayani Urambo alichukua pikipiki ya marehemu aina ya Sanlg na kuondoka nayo hadi Usinge wilayani Kaliua na baadae alikamatwa na Polisi na kuhojiwa kisha akaeleza tukio zima la mauaji aliyoyafanya na kuonesha eneo ambalo mwili wa marehemu alipokuwa ameuchimbia shimo na kuufukia.
Katika Shauri hilo la Mauaji namba 19 la mwaka 2019 ambalo lilisikilizwa na Hakimu mwenye mamlaka ya ziada katika Mahakama ya Hakimu mkazi Mkoa wa Tabora, Beda Nyaki alipitia maelezo ya pande zote mbili na kujiridhisha pasipo shaka kwamba mshitakiwa UKENYENGE ushahidi wa kimazingira umemuhusisha moja kwa moja kwamba alitenda mauaji hayo kinyume na kifungu cha 196 sura namba 16 kanuni ya adhabu.
You must be logged in to post a comment.