Kipa chaguo la kwanza katika kikosi cha Tanzania Prisons, Jeremia Kisubi anahesabu siku tu kabla ya kutua Jangwani ili kuitumikia Yanga

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Yanga ambazo tulizipata jana asubuhi ni kwamba meneja wa mchezaji huyo alikutana na uongozi wa Yanga.

Meneja wa Kisubi asubuhi ya leo, alikwenda katika ofisi za GSM na kufanya kikao kilichokuwa kirefu juu ya mazungumzo ya kumuachia mchezaji wake.

“Muda huu hapa ndio wametoka kuzungumza meneja wa Kisubi pamoja na Injinia Hersi Said jinsi ya kumpata kipa huyo ili msimu ujao aweze kuitumikia Yanga,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya Yanga.

“Kimsingi mazungumzo yamekwenda vizuri kati ya mwakilishi wa mchezaji pamoja na Hersi na halitakuwa jambo la kushangaza Kisubi kusaini mkataba wa miaka miwili ambao wamekubaliana.

“Tumepanga kulifanya hili kimyakimya na kama tukifanikiwa kumpata, maana yake tutaboresha eneo la makipa wetu watatu kwa kuachana na mmoja.”

Baada ya kikao hicho cha mwakilishi wa mchezaji na Hersi kusichopungua dakika 30, walikubaliana na kazi imebaki kwa Yanga kulipa stahiki zote ili Kisubi asaini mkataba na kutangazwa.