Kafanyeni Tohara kupunguza maambukizi ya virusi vya ukimwi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Selemani Jafo amewataka wanaume ambao hawajafanyiwa tohara katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara nchini kuhakikisha wanajitokeza kufanyiwa Tohara ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi nchini

Akizindua magari kwa ajili ya utoaji wa huduma tembezi za Tohara (Maounted mobile Clinic Vans) kwa wanaume leo katika Ofisi za Rais –TAMISEMI, mtumba jijini Dodoma Waziri Jafo amesema kuwa kunafaida kubwa kwa wanaume kufanyiwa tohara.

“Wale ambao hawajapata Twahara, waende wakapate Twahara kwa kuwa uwekezaji huu mkubwa umekuja kwenu, kupata Huduma tembezi za Tohara ni fursa ya kipekee sana, haijawahi kutokea katika maeneo mengine, tumieni fursa hiyo” amesema Waziri Jafo

Waziri Jafo anaendelea kufafanua kuwa ipo mikoa 16 ambayo inachangamoto kubwa ya maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi kutokana na watu kukosa kufanyiwa tohara,hivyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kujikinga na maambukizi ya ukimwi nchini.

Amesema kuwa kutokana na taarifa za wataalam zinavyosema kuwa wale ambao wamepata tohara wanaasilimia kubwa ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa asilimia 60

“Tohara inasaidia kupunguza magonjwa ya kuambukiza yanayoendana na ngono kama kaswende lakini pia inaonekana wazi kwamba waliofanyiwa tohara wanapata nafuu nyingi sana katika suala la afya na mazingira yao” anafafanua Waziri Jafo

Amewaagiza waganga wakuu wa Mikoa na Halmashauri katika Mikoa iliyopatiwa magari kufanya uratibu mzuri kwa kupanga vizuri jinsi magari hayo yatakavyofanya kazi na kuwasaidia wananchi.

Amewataka kuhakikisha wanalinda na kutunzwa kwa magari na vifaa vyake, kwa kuwa yamenunuliwa kwa gharama kubwa hivyo ni vyema vikatunzwa na kufanyiwa kazi iliyokusudiwa kwa jamii.

“Si tarajii hata kidogo siku ninatembelea mikoa hiyo nakutana na kitanda kimetolewa kwa matumzi mengine,taa zimetolewa na wanafanya upasuaji kwa tochi ya simu, sitarajii vifaa vingine ambavyo vimefungwa ndani ya gari kungolewa na kutolewa” amesisitiza Waziri Jafo

Amewaagiza Makatibu Tawala kuhakikisha wanasimamia fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ununuzi wa Dawa na kuwataka waganga wakuu wa Mikoa kuhakikisha wanasiamamia upatikanaji wa Dawa katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya katika maeneo yao.

Aidha,amewaagiza wakurugenzi kuhakikisha hakuna wananchi wanaolalamika kuhusu ukosefu wa dawa kwenye vituo vyote vilivyoko katika maeneo yao.

Wakati huohuo, Mkurugenzi Mkazi Interhealth International Dkt. Lucy Raymond amasema wanaume zaidi ya 1,820,000 wamepatiwa huduma ya Tohara na watumishi 1,000 wa afya wamepatiwa mafunzo ya utoaji huduma bora za tohara, usimamizi wa ubora na uhifadhi wa takwimu tokea mwaka 2010 hadi sasa.

Dkt. Lucy amesema magari ambayo yatatumiwa kwa ajili utoaji huduma tembezi za Tohara yamenunuliwa kwa ufadhili wa mfuko wa Rais wa Marekani wa kupambana maambukizi ya Virusi vya ukimwi yanavifaa vyote muhimu vya utoaji huduma ya tohara pamoja na huduma nyingine zikiwemo upasuaji mdogo, uchunguzi wa magonjwa yasiyo ambukiza na vifaa tiba vya huduma za dharura vimewekwa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma bora hususani katika maeneo ya pembezoni yasiyo fikika kirahisi.

Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI