Mkuu wa mkoa wa Mara, Mh. Adam Malima amesema kuwa Mkoa wa Mara unatarajia kuanza uzalishaji wa zao la mkonge huku lengo likiwa ni kuvuna tani 20,000 kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitano ijayo mkakati unaokwenda sambamba na ule wa Taifa unaolenga kuboresha kilimo hicho na kuongeza mavuno kutoka tani 38,000 za sasa hadi tani120,000 katika kipindi hicho.

Mh. Malima amesema kuwa zao hilo la mkonge limetambulishwa rasmi kama zao la fursa kwa wakazi wa mkoa wa huu ambapo amsema kuwa zao hilo litasaidia kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na mkoa kwa ujumla kutokana na mahitaji yake katika soko la dunia.
Amesema kuwa kilimo cha zao hilo ni mwendelezo wa maono ya serikali ya mkoa ya kutaka kuboresha uchumi wa mtu mmoja mmoja kupitia kilimo na kwamba mbali na mkonge mazao ya Kahawa na Pamba pia ni miongoni mwa mazao ya kimkakati yanayotarajiwa kutumika kufanya mapinduzi ya kilimo na uchumi ndani ya mkoa.
Mh. Malima alisema kuwa uamuzi wa kuanzisha kilimo cha zao la mkonge mkoani Mara unatokana na utafiti uliofanywa na kubaini kuwa zao hilo linaweza kustawi na kuwa na mavuno mazuri endapo wakulima katika halamshauri tano za mkoa huo watapata mafunzo juu ya kilimo bora cha zao hilo.
Amesema kuwa ili kufanikisha lengo jilo tayari mkoa imeanza mikakati mbalimbali itakayowezesha zao hilo kulimwa kwa tija ambapo miongoni mwa mikakati hiyo ni kuwa na maafisa ugani angalau 60 wenye utaalam wa kilimo hicho ambapo tayari utaratibu unafanyika ili waweze kupewa mafunzo ya muda mfupi juu ya utalaam wa zao la mkonge.
Mh. Malima amesema kuwa kwa kuanzia mkoa unatarajia kuwa na ekari 6,000 za zao hilo huku malengo ya muda mrefu ni kulima ekari 20,000 na kwamba ili kufikia malengo hayo wakulima watapewa miongozo kwa ukaribu zaidi ili kilimo kiweze kuwa njia mojawapo ya uhakika ya kupunguza umasikini kwa wananchi.
You must be logged in to post a comment.