Serikali imesema imechukua hatua za kutumia ndege kunyunyiza viuatilifu (sumu) ili kuua makundi ya nzige wa jangwani ambao wamevamia maeneo ya Wilaya za Simanjiro na Longido na kuhatarisha ustawi wa mazao na malisho ya mifugo kwenye maeneo hayo.
Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda ametembelea eneo la Wilaya ya Longido ambalo limevamiwa na nzige wa jangwani ambapo amesema kuwa kuanzia leo ndege maalum itafanya kazi kupulizia viuatilifu kuua nzige hao.
Prof. Mkenda amewaeleza Wananchi na Viongozi kuwa wasiwe na hofu nzige wote watadhibitiwa kupitia Wataalamu wa Wizara ya Kilimo waliopo kwenye maeneo yote yenye dalili za uwepo wa wadudu hao nchini.