Karibu katika mwanzo wa kipindi cha Toba na tafakari! Leo sisemi kwa maneno mengi, ila nawapa simulizi hii ya kweli kisha utaamua.
Simulizi inaanzia mwaka 1953, kijana mdogo, Joseph Ligoni, akiwa na umri wa miaka 15, aliposhutumiwa na kuhukumiwa kushirikianaa na kikundi cha vijana walevi, waliofanya ujambazi na kugharimu uhai wa watu wawili huko Philadelphia, Nchini Marekani. Akiwa kijana mdogo, anahukumiwa kama mfungwa mtoto (juvenile) kifungo cha maisha jela.
Ligon aliendelea kusimamia msimamo wake kuwa, siku hiyo hakuhuska na jinai yoyote, licha ya yote na kutokuwa na hatia anaingia Gerezani bila haki ha kupokea msamaha wa mapema yaani Parole, haki inachelewa zaidi. Mwaka 2017, Ligoni alipunguziwa adhabu, akapewa haki ya kupokea msahamaha wa mapema yaani kupunguziwa adhabu, Ligoni mzee sasa anakataa, na alipoulizwa kwa nini akatae nafasi hiyo, anajibu kuwa Parole si uhuru ila ni kukubali hatia na kukiri kubadilika ili upunguziwe adhabu, na yeye hana hatia hivyo huo kwake haukuwa uhuru bado.
Mawakili wa Kituo kinachohusika na utetezi wa makosa ya jinai kwa watoto (YSRP) waliendelea kutetea haki yake, mwaka huu 2021, Logan akiwa na miaka 83, hatimaye wakili anafanikiwa kuishawishi mahakama kumfutia hatia Ligoni, na Alhamisi ya tarehe 11,Ligoni anatoka nje ya Gereza na anapookelewa na Kituo cha YSRP kama familia yake. Anatoka hana familia, marafiki wala ndugu wa karibu tena. Katika uzee wake hana mke wala mtoto. Sasa anatajwa kama Mfungwa nambari mbili kati ya wafungwa waliowahi kutoka gerezani wakiwa hai baada ya kutumikia kifungo cha muda mrefu zaidi. Mwisho wa simulizi yetu ya ukweli.
Ndugu, leo nawaandikia haya, kwani naona wapo wakristo hawaoni haya kusingizia na hata kutoa ushahidi wa uwongo ali mradi tu fulani adhurike, kijana wangu mmoja alikuwa mahala fulani anatoa semina, basi simu kadhaa badae anletewa kesi kuwa alivaa vazi la Misa, Kanzu nyeupe wakati wa semina hiyo, anatahamaki na kushangaa namna anahukumiwa kwa kosa ambalo hajafanya na hta mashuhuda wanakiri wazi hakuvaa na hawajapata kumwona, ikatafutwa picha za miaka iliyopita, kijana wangu alipiga hali anajiandaa kuongoza ibada ya Njia ya msalaba, inawekwa kama ushahidi, yote ni kumtafutia hatia. Lakini anafanikisha kusema kuwa hakuvaa. Wapo waamini walei wafitinishaji kazi yao kuchonganisha viongozi na Mapadre, mapadre na Mapadre, waamini kwa waamini, yeye ndio furaha yake.”Usivumishe habari za uongo; usitie mkono wako pamoja na mwovu, kuwa shahidi wa udhalimu.” Kutoka 23:1. Lakini utapata nini ikiwa ndugu yako atapoteza kazi yake, ndoa yake, amani, haki na hata maisha, je utaongezewa wewe haki hiyo au mshahara? Hebu fikiri washitaki wa Ligoni walipata faida gani baada ya Ligoni kupoteza ndoto zake? Au wahukumu wa kijana wangu walipata faida gani alipokasirishwa na kusononeka kwa shutuma za wongo, walimama wao katika nafasi yake?
Ndugu zangu, Mungu wetu ni wa haki, hapendezwi na mtu atoaye ushahidi wa uongo dhidi ya wengine.
“Kuna vitu sita anavyovichukia BWANA;
Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya kiburi, ulimi wa uongo,
Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia;” Mithali 6:16-17 “Nami nitawakaribieni ili kuhukumu; nami nitakuwa shahidi mwepesi juu ya wachawi, na juu ya wazinzi, na juu yao waapao kwa uongo; na juu yao wamwoneao mwenye kuajiriwa, kwa ajili ya mshahara wake, hawaniogopi mimi, asema BWANA wa majeshi.” Malaki 3:5.
Basi kwenu wenye kuamua, Bwana anakumbusha hivi
” nao waamuzi na watafute kwa bidii; na tazama, yule shahidi akiwa shahidi wa uongo, naye ametoa ushahidi wa uongo juu ya nduguye;” Torati 19:18.
Mwisho nakusihi acha fitina, wivu wa ajabu ajabu, lakini ikumbuke Amri ya nane, Usiseme Uongo. Usitoe ushahidi wa uongo, usisem jambo kama huna hakika. Watu wanaumizwa kwa maneno ya uongo au kukosa hakika. Acha umbea umbea mara fulani mchawi, mara yule hivi! Hakika huna, tulia Mkristo unafanya chukizo, ni muda wako kurekebisha mahusiano uliyoharibu kwa kusema wongo, kaombe na radhi kwao!
Tumshukuru Yesu Kristo.
Nawatakia wakati mwema, tujikinge na Korona na tusieneze taarifa za uongo au ambazo hazina uhakika kuhusu ugonjwa huu.