
Mbunge wa Jimbo la Mbagala Mhe. Abdallah Chaurembo jana Jumapili 14, Februari 2021 amewataka wananchi wa Mtaa wa Malela uliopo Kata ya Toangoma kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo katika Mtaa huo.
Hatua hiyo imekuja baada ya malalamiko ya wananchi hao juu ya upatikanaji wa huduma mbalimbali zikiwemo barabara, umeme, maji n.k
Akizungumza wakati wa Mkutano huo Mhe. Chaurembo aliwasisitiza wananchi hao juu ya umuhimu wa kuchangia shughuli za maendeleo ya Mtaa huo.
“Nimesikia na kuzipokea changamoto zote mlizozitaja zikiwemo za barabara, umeme, maji n.k” alisema Chaurembo.
“Kabla ya kuendelea kuzungumza naomba kuwauliza wananchi wenzangu, Serikali ni nani?, jibu ni wewe,mimi na yule, kwa hiyo inatupasa kuchangia shughuli za maendeleo kuliko kuitegemea Serikali kuu pekee” alisema Chaurembo.
“Mtakapoanza kuchangia shughuli za maendeleo na kukidhi viwango vya kuweza kupata fedha za Jimbo, nitazielekeza huku kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya miradi hiyo mtakayoianzisha” alisema Chaurembo.
Sambamba na hilo Mhe . Chaurembo amepongeza zoezi la urasimishaji linaloendelea katika Mtaa wa Malela, ambalo lilianza mwezi Septemba, 2020 na sasa tayari hati zimeanza kuandaliwa.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Toangoma Mhe. Mketo aliwataka wananchi hao kushirikiana na Ofisi ya Serikali ya Mtaa wao ili kuweza kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Mtaa wa Malela Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo ndg. Oswin Mkinga alimshukuru Mhe. Chaurembo kwa kuweza kufika katika Mkutano huo.
“Tunakushuru Mbunge, Mhe. Chaurembo kwa kuweza kufika katika Mkutano wa Mtaa wetu,sambamba na hilo tumefurahi jinsi ulivyozipokea changamoto zetu na ulivyoshauri namna ya kuzitatua baadhi ya changamoto hizo” alisema Mwenyekiti Oswin.
“Pia naomba nikupe taarifa Mhe. Chaurembo kwamba Mtaa wa Malela ndiyo Mtaa pekee ambao umeendesha zoezi la urasimishaji kwa haraka na ufanisi ndani ya muda mfupi, hati 110 zinaanza kulipiwa Jumatatu 15 Februari 2021” alisema Oswin.
Katika Mkutano huo Mhe. Chaurembo alifatana na Diwani wa Kata hiyo Pamoja na Katibu wa Siasa na Uenezi Wilaya ya Temeke Ndg. Ally Mussa Kamtande, ambaye licha ya kuwashukuru wananchi wa Mtaa wa Malela kwa kuipigia CCM kura nyingi za ndio kwa pamoja walikata cake ya Valentine’s iliyoandaliwa na Serikali ya Mtaa wa Malela na kuwalisha wananchi baada ya kumalizika mkutano ikiwa ni ishara ya upendo mkubwa kwa wananchi wa Malela.
Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Mbagala
Malela, Toangoma.
You must be logged in to post a comment.