Seneti yashindwa kutimiza theluthi mbili iliyohitajika kumtia hatiani Trump

Bunge la Seneti nchini Marekani limeshindwa kutimiza akidi ya theluthi mbili iliyohitajika ili kumtia hatiani rais wa zamani Donald Trump kutokana na madai ya kuchochea vurugu katika jengo la Capitol tarehe 6 mwezi Januari.

Maseneta walio wengi 57 kwa 43, wakiwemo saba wa chama cha Republican- walipiga kura kumhukumu Bw. Trump, kura 10 zaidi zilihitajika kumtia hatiani.

Baada ya kushindwa kumtia hatiani, Bw. Trump alilaani kesi hiyo akiita ”kesi ya kumtafuta mbaya”. Hii ni kesi ya pili dhidi ya Trump.

Kama angetiwa hatiani, bunge la seneti lingepiga kura dhidi yake kumzuia kuwania nafasi hiyo tena.

Baada ya kura, Seneta mwandamizi wa chama Republican ndani ya Congress Mitch McConnel alisema Trump amekuwa ”akiwajibika” kutokana na kile kilichotokea Capitol.

Awali, alipiga kura dhidi ya kutiwa hatiani kwa Trump, akisema hatua hiyo ni kunyume cha katiba kwa kuwa Trump si rais tena. Bw.McConnell amekuwa akipinga vikali kesi dhidi ya Trump mpaka alipoondoka madarakani tarehe 20 mwezi Januari.

Hata hivyo Bw McConnell alimtahadharisha Trump kuwa bado anaweza kuwajibishwa mahakamani.

”Si kwamba amekwepa chochote. Tuna mfumo wa kushughulikia jinai katika nchi hii, tuna mashtaka ya raia na marais wa zamani hawana kinga ya kutowajibishwa,” alisema.

Rais Joe Biden alisema: ”Wakati kura ya mwisho haikuwezesha Trump kutiwa hatiani, kiini cha mashtaka hakina ubishi.

”Hatua hii ya kusikitisha katika historia yetu imetukumbusha kuwa demokrasia iko hatarini. Na kuwa wakati wote lazima ilindwe.

Kuwa ni lazima kuwa macho.Vurugu na msimamo mkali havina nafasi nchini Marekani. Na kuwa kila mmoja wetu ana kazi na wajibu kama Wamareani na hasa kama viongozi, kutetea ukweli na kuushinda uongo.”

Katika kuhitimisha , bunge la wawakilishi wa Democratic walisema itakuwa ni hatari kumuachia Bw. Trump

”Hatari inaweza kuwa kubwa kwa kuwa ukweli mchungu ni kuwa kile kilichotokea tarehe 6 mwezi Januari kinaweza kutokea tena mwakilishi Joe Neguse alisema.

Hatahivyo, wakili wa Bw. Trump, Michael van der Veen, ameita kesi hiyo ”maonesho” na kusema kuwa Democrat ‘walikuwa wanafanya hila” kumshtaki Bw.Trump

“Kesi hii imekuwa maigizo kutoka mwanzo hadi mwisho,” alisema. “Maonesho yote hayajawa chochote isipokuwa harakati isiyo na dhamana na hila za kisiasa za muda mrefu dhidi ya Bw Trump na chama cha upinzani.”

Trump mwenyewe amesema hakuna rais ”aliyewahi kupitia hatua kama hii na kuwa ” harakati za kuifanya Marekani kuwa kubwa tena” ndio kwanza zimeanza”. 

Awali Maseneta walipiga kura kwa ushuhuda binafsi, ambao ungechelewesha uamuzi wa Jumamosi. Lakini baada ya mashauriano ya dharura walibadilisha uamuzi wao kukubali taarifa zilizoandikwa tu.