Klabu Bingwa Afrika: Simba imepata ushindi jijini Kinshasa miaka miwili baada ya kukubali kichapo cha 5-0 dhidi ya Vita.

Simba yaanza hatua ya makundi kwa ushindi dhidi ya AS Vita Kinshasa

Mambingwa wa Tanzania Simba SC wameanza hatua ya makundi kwa ushindi wa ugenini wakiitungua AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kwa goli 1-0.

Goli la Simba lilipatikana katika dakika ya 61 likiwekwa wavuni na mshambuliaji raia wa DRC Chris Mugalu kupitia mkwaju wa penati.

Goli la Simba katika mchezo huo uliopigwa Ijumaa usiku katika dimba la Mashahidi jijini Kinshasa lilipatikana katika dakika ya 61 likiwekwa wavuni na mshambuliaji raia wa DRC Chris Mugalu kupitia mkwaju wa penati. Simba walipata penati hiyo baada ya shambulizi kali lililofanywa na viungo Clatous Chama na Luis Miquissone ambalo lilizuiwa kwa mkono na beki wa Vita Ousmane Outtara katika eneo la hatari. 

Ushindi wa Simba unakuja miaka miwili kamili toka walipofungwa goli 5-0 na AS Vita katika hatua ya makundi ya mashindano hayo msimu wa 2018/19. Hata hivyo Simba iliwafunga Vita 2-1 katika mchezo wa marudiano uliofanyika jijini Dar es Salaam. 

Simba ilionesha ukomavu na umakini wa hali ya juu katika safu ya ulinzi katika mchezo wa jana ikilinganishwa na kilichotokea jijini Kinshasa miaka miwili iliyopita. Kwa ujumla wake, Vita ilimiliki mchezo kwa asilimia 55 na kufanya mashambulizi mengi zaidi lakini safu ya ulinzi ya Simba iliweza kuhimili vishindo vya wapinzani wao.

Mechi ya jana ndio imefungua pazia la Kundi A na mchezo unaofuatia wa kundi hilo baina ya miamba ya Misri na mabingwa watetezi wa Klabu Bingwa Afrika Al Ahly na miamba ya Sudani Al-Merrikh utapigwa siku ya Jumanne jijini Cairo. 

Mchezo unaofuata kwa Simba utakuwa dhidi ya Al Ahly katika dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam mnamo Februari 23. Timu hizo mbili pia zilikutana katika hatua ya makundi msimu wa 2018/19 na mchezo wao wa mwisho Februari 12, 2019 Simba iliibuka na ushindi wa goli 1-0 jijini Dar es Salaam. Awali Simba ilikubali kichapo cha goli 5-0 jijini Cairo Februari 2, 2019. 

Simba ina rekodi nzuri jijini Dar es Salaam toka msimu wa 2018/19 wa kutokupoteza mechi yoyote nyumbani na endapo wataandikisha ushindi dhidi ya Al Ahly watakuwa wamejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa hatua inayofuata ya robo fainali. 

Jana pia umepigwa mchezo mmoja mwengine wa michuano hiyo wa kundi D baina ya Zamalek ya Misri na MC Alger ambao uliisha kwa sare ya 0-0 licha ya wenyeji Zamalek kuutawala mchezo huo kwa asilimia 76. Michezo mitano ya michuano hiyo ina inatarajiwa kupigwa hii leo.