Fahamu msingi wa kuwekwa ukomo wa madaraka Kikatiba

Nchini Tanzania, umeibuka mjadala ndani ya Bunge kuhusu umuhimu wa kubadili Katiba ili Rais John Magufuli aruhusiwe kuongoza kwa kipindi kingine. Katiba ya Tanzania inaruhusu Rais kukaa madarakani kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano. 

Rais Magufuli mwenyewe amewahi kuzungumza hadharani kwamba hana nia ya kuendelea kubaki madarakani baada ya kumaliza muda wake wa kikatiba. Muda wake unamalizika rasmi mwaka 2025 baada ya kufanikiwa kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2015 na 2020.

Hata hivyo, pamoja na maneno hayo ya Rais, bado wabunge na wanasiasa wengine wamekuwa wakitoa kauli zenye mwelekeo huohuo wa kutaka Katiba ibadilishwe ili ukomo huo wa kubaki madarakani uondolewe.

Tanzania si nchi ya kwanza barani Afrika kuwa na mjadala wa aina hii ndani na nje ya Bunge. Tangu nchi nyingi za bara hili zilipoamua kuingia katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi mwanzoni mwa miaka ya 1990, muongo mmoja uliopita umeshuhudia mataifa mengi yakipiga hatua nyuma kwenye suala la kuheshimu ukomo huo wa kikatiba.

Kuanzia kwa Burundi ya Pierre Nkurunziza, Uganda ya Yoweri Museveni, Togo ya Faure Gnassingbe, Rwanda ya Paul Kagame na Jamhuri ya Congo ya Dennis Sassou Ngueso, hali imekuwa ya kufanana.

Maswali ambayo yamekuwa yakiulizwa katika duru za kisiasa ni yafuatayo; nini maana ya mienendo hii? Kuna umuhimu wa kuwa na ukomo wa viongozi kukaa madarakani? Na je, sababu zilizosababisha kuwepo kwa ukomo miaka ya nyuma bado zina maana hadi leo? 

Kwanini ukomo uliwekwa kwenye Katiba za nchi mbalimbali?

Utaratibu wa kuweka ukomo wa viongozi kubaki madarakani una asili yake nchini Marekani. Nchi hiyo ambayo ndiyo kinara wa mfumo wa dunia baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, ilifanya hivyo mwaka 1951.

Walioamua kufanya hivyo walifuata nyayo za viongozi wawili mashuhuri wa zamani wa taifa hilo, George Washington na Thomas Jefferson, ambao waliongoza kwa vipindi viwili na hawakuona umuhimu wa kuendelea hata kama Katiba yao wakati wao haikuwa ikiwakataza.

Ni muhimu pia kufahamu kwamba Marekani – kwa asili, ni taifa linalopinga mambo ya utawala wa kifalme na hivyo kitendo cha kuwa na Rais anayekaa madarakani kwa muda mrefu kinaweza kuweka hatari ya kuonekana au kujiona kama mfalme.

Walioweka vifungu hivyo kwenye Katiba ya Marekani walijiridhisha kwamba jambo ambalo kiongozi atashindwa kulifanya ndani ya miaka minane madarakani, hawezi kulifanya hata akiongozewa muda kiasi gani.

Tabia hiyo ya Wamarekani ni tofauti na ile ya Wachina. China, ingawa lilikuwa taifa kubwa na imara kabla ya Marekani, halikuweza kuweka misingi ya ukomo wa vipindi vya kutawala hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Tofauti ya Marekani na China ni kwamba wakati hofu kuu ya Wamarekani ilikuwa ni kwenye Ufalme, kiongozi wa China kwenye miaka ya 1980, Deng Xiaoping, hakutaka taifa hilo lije kuongozwa na utawala wa Kiimla kama wa Mao Zedong, na ndiyo sababu wakaamua kuweka utaratibu na namna ya kuufuata.

Inajulikana kwamba pamoja na kuweka mifumo hiyo, zimekuwapo sauti za kutaka kubadili utaratibu huu wa ukomo ndani ya Marekani na China pia. Mwaka 1987, kulikuwapo na kikundi cha Wamarekani waliotaka Katiba ibadilishwe ili aliyekuwa Rais wakati huo, Ronald Reagan, aendelee kubaki madarakani.

China pia ilikuwa na upinzani wa chinichini kuhusu utaratibu huo na sasa inaonekana Rais XI Jinping wa China anaenda kuwa Rais wa kwanza wa China atakayekuwa na umri zaidi ya miaka 68 – kinyume na matakwa ya Katiba yao.

Bunge la Tanzania

Utafiti uliofanywa na Dulani katika nchi tofauti 34 za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, ulionyesha kwamba asilimia 73 ya waliohojiwa walipendelea utaratibu wa kuwa na ukomo wa kukaa madarakani. Hii maana yake ni kwamba Waafrika wanapenda viongozi wao kubadilika.

Kuna sababu kadhaa za umuhimu wa kubadili viongozi. Mabadiliko huleta watu wenye maono tofauti kuhusu masuala mbalimbali, kutoa fursa ya watu wa dini, makabila, asili, jinsia na rangi tofauti kupata fursa ya kukaa madarakani na pia – wakati mwingine, kugawa sawia keki ya taifa.

Katika nchi nyingi zinazoendelea hususani zile za Afrika, mtu anayekuwa madarakani mara nyingi hutoa fursa za kiuchumi kwa watu wa asili yake, marafiki zake au watu anaojuana nao. Hii maana yake ni kwamba kuwa na Rais wa jamii ni fursa kwa watu wa karibu.

Amani na utulivu ndani ya nchi na chama chake vinaweza kudumu kwa kuwa tu watu wa asili nyingine na makundi mengine wanajua kwamba itafika hatua ‘mtu wao’ ataingia madarakani na hivyo huo nao utakuwa wakati wao wa kufaidi mema ya nchi. 

Tanzania, kwa mfano, imewahi kuwa na marais watano kutoka katika maeneo tofauti ya nchi hiyo – wakiwa na makabila na dini tofauti na hilo likielezwa kuwa mojawapo ya mambo yanayolifanya taifa hilo kuwa na Amani na utulivu kulinganisha na majirani zake.

Kwa sababu hiyo, ukomo wa kikatiba wa muda wa viongozi wakuu kuhudumu katika nafasi za juu ni muhimu kwa sababu unasaidia kujenga umoja wa kitaifa na kuweka dhana kwamba nchi ni ya wote na si ya watu wa kabila, kundi, dini au imani fulani.

Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kuzungumza wakati fulani kwamba wakati alipokuwa akiwaambia baadhi ya wasaidizi wake kuwa anataka kuachia ngazi wengi walikuwa wakimkatalia kwa maelezo kwamba nchi ilikuwa changa. Hata hivyo, kwa utani, Mwalimu alisema ambacho hakujua ni kuwa wasaidizi wake wale walikuwa wakizungumzia uchanga wa familia zao na si nchi. 

Mwalimu alimaanisha kuwa wasaidizi wake walijua wataendelea kufaidi ali mradi Nyerere akiendelea kuongoza nchi. Mabadiliko ya kuja kwa mtu mwingine yangemaanisha wao kutoka na nafasi zao kuchukuliwa na wengine. Hiyo ndiyo sababu ukomo wa kukaa madarakani kikatiba ni muhimu.

Nini maana ya kelele hizi za mara kwa mara?

Uzoefu wa Tanzania na katika nchi nyingine unaonyesha kwamba kelele za kutaka kubadili Katiba hupigwa na watu wa aina mbili; wale wanaofaidika na utawala uliopo na wale ambao wanajipendekeza kwa watawala. 

Tatizo la kubadili Katiba kufaidisha viongozi linaonekana kubwa zaidi barani Afrika kwa sababu tu nyingi ya taasisi za usimamizi wa demokrasia bado ni changa na dhaifu. Iliichukua Marekani miaka 150 ya kuwa kama nchi kuweka utaratibu na misingi ya kuheshimu Katiba.

Nchi nyingi huru za Afrika na zinazoendelea hazina hata miaka 100 ya kuwa nchi huru na urahisi wa kucheza na Katiba husababishwa zaidi na udhaifu huo.

Hata hivyo, kuna jambo moja ambalo liko dhahiri; ziko nchi za Afrika ambazo mfumo na utaratibu wa kubadilishana viongozi umeanza kushika mizizi kiasi kwamba ni vigumu sana kurudi nyuma. Nchi hizo ni kama vile Ghana, Senegal, Tanzania, Afrika Kusini, Botswana, Nigeria na Mauritius.

Kuna nchi nyingine kama Uganda, Rwanda, Zimbabwe na nyinginezo ambapo viongozi waliopo madarakani hawakuingia madarakani kwa mara ya kwanza kwa njia za kistaarabu. Kuna ambao ilibidi waingie msituni kupigana vita na inaonekana imani yao kwa sanduku la kura haiko thabiti.

Marekani walijaribu kutaka kubadili Katiba ili Reagan awanie tena urais takribani miaka 40 tu baada ya kuweka ukomo. Inawezekana pia kwa nchi ambazo tayari zimeshakuwa na tabia ya kubadilisha viongozi, kuingia katika kutaka kubadili lakini huwa haiwi kazi rahisi kwa vile huo tayari unakuwa ni utamaduni.

Wachambuzi wengi wa kisiasa wanaamini kwamba mara baada ya kiongozi wa kwanza aliyechaguliwa kwa kura kukubali kufuata Katiba na kumwachia mwingine na huyo mwingine akafanya hivyo – kwa maana ya mara tatu; mara nyingi mfumo unakuwa umeshazoea.

Hii ni kwa sababu, mara nyingi muda wa kukaa madarakani ni kati ya miaka minane hadi kumi na hivyo inapokuwa mara tatu maana yake ni kwamba kizazi kizima kinakuwa kimezoea hali hiyo. Ni vigumu kufanya jambo na kufanikiwa wakati kizazi kilichopo hakijazoea jambo hilo.

Mjadala huu kuhusu ukomo utaendelea kuwepo kwa muda mrefu wakati nchi na mataifa mbalimbali yakijaribu kutafuta njia zake zenyewe za kujiongoza. Hata hivyo, kwa nchi ambazo zimeamua kufuata mfumo wa Jamhuri (Republic), ni vigumu kuachana na utaratibu wa kuweka ukomo wa kikatiba.

Kwa nchi ambazo viongozi wake waliingia madarakani kwa mtutu wa bunduki na hawajawahi kushuhudia viongozi wakipishana madarakani kwa sanduku la kura, safari yao bado ni ndefu.