Halmashauri zatakiwa kufanya Msawazo wa Walimu

OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imeziagiza Halmashauri zote nchini kufanya msawazo wa walimu wa Shule za Msingi na Sekondari kwa kuzingatia jinsia.

OR-TAMISEMI, Bungeni Dodoma

Aidha, Serikali ipo kwenye mpango wa mwisho wa kutoa ajira mpya kwa walimu.

Akijibu swali bungeni leo la Mbunge wa Viti maalum(CHADEMA),Kunti Majala, aliyetaka kujua serikali itapeleka lini walimu wa kike katika Shule za Msingi Birise na Donsee ambazo hazina walimu wa Kike, Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, David Silinde, amesema serikali imeendelea na utaratibu wake wa kuajiri walimu mara kwa mara.

Amesema kwasasa serikali ipo kwenye mpango wa mwisho wa kutoa ajira mpya kwa walimu na suala hilo litazingatiwa jinsia ili kuwasaidia watoto wa kike nchini.

“Serikali inatambua tatizo la ukosefu wa walimu wa kike katika Shule za Msingi Birise na Donsee zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Mkoa wa Dodoma,”amesema.

Hata hivyo, amesema katika kukabiliana na tatizo hilo Halmashauri ya Wilaya ya Chemba imempeleka mwalimu mmoja wa kike katika Shule ya Msingi Donsee wakati ikiendelea kukamilisha taratibu za kumpeleka mwalimu wa kike katika Shule ya Msingi Birise.

Mwisho.