WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Wakala wa Barabara mijini na Vijijini (TARURA) kwa ujenzi imara wa barabara Jamhuri na Msikiti wa Gadafi, yenye urefu wa kilomita 1,
Pia ametoa miezi 5 kukamilishwa kwa ujenzi wa barabara ya Nkuhungu-JCT Chamwino yenye urefu wa kilomita 1, inayokarabatiwa kwa kiwango cha lami nyepesi.
Jafo alitoa pongezi hizo leo jijini Dodoma mara baada ya kukagua ujenzi wa Barabara hizo.
Amesema ameridhishwa na ujezi wa barabara ya lami nzito uliotekelezwa na Mkandarasi Nyanza Road kwa Gharama ya Sh bilioni 1.072 kwa muda wa siku 60, huku akihimiza kuimarisha usafi wa mitaro ya barabara hiyo.
“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya mimi hapa sina nongwa kabisa, nimeridhika na ujenzi huu na hasa ikizingatiwa kwamba eneo hili yanapita magari yenye uzito tofauti tofauti yakiwepo malori, hivyo kujenga kwa kiwango hiki cha lami nzito ilikuwa ni sahihi kabisa”
Akiwa katika eneo la Barabara ya Nkuhungu- JCT Chamwino, Jafo, alitaka kujua muda sahihi uliopangwa kukabidhi kazi hiyo ambayo imesita kwa muda kutokana na hali ya hewa.
Awali, Mhandisi wa TARURA Mkoa Lusako Kilembe, alimwambia Mhe. Waziri, kazi hiyo inatazamiwa kukabidhiwa mwezi wa sita hatua iliyomlazimu Waziri kutoa maelekezo ya kuharakishwa kwa kazi.
“Mtendaji mkuu wa TARURA, huyu Mhandisi, msije mkamhamisha hapa anaonekana ni mtu anayefahamu vema majukumu yake na hasa kwa mahitaji ya Makao Makuu ya Nchi, nitoe rai tu, kufikia mwezi Juni kwa tarehe iliyopangwa kazi hii iwe imekamilika.”
Barabara ya Nkuhungu JCT Chamwino inajengwa kwa gharama ya Sh milioni 819.4, ambapo ujenzi wake unategemea kuchukua siku 180 hadi kumalizika.
Mhandisi Lusajo, aliahidi muda uliobakia ambao ni siku siku 140 wakati maendeleo ya mradi huo umefikia asilimia 10 ya mradi mzima.
Akisoma taarifa ya ujenzi, Mhandisi wa TARURA, Mkoa wa Dodoma Lusako Kilembe, alisema changamoto kubwa iliyoathiri mradi kutokamilika kwa wakati ni mvua zinazoendelea kunyesha mfululizo mkoani hapo.
Barabara ya Nkuhungu JCT Chamwino, inajengwa na Mkandarasi G’s Contractors Co. Ltd ya mkoani Iringa, ambapo urefu wa barabara ni Kilomita 1 inayojengwa kwa kiwango cha lami nyepesi, ujenzi wa mifereji ya maji, mita 300 ujenzi wa kalvat 8 na uwekaji wa alama za barabarani.
Waziri Jafo, alikuwa katika ziara za kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na wakala wa Barabara Mijini na Vijijini TARURA mjini Dodoma.
Na Atley Kuni, Dodoma


You must be logged in to post a comment.