Upande wa Jamhuri katika shauri la ubakaji namba 55 la mwaka 2020 umefunga ushahidi dhidi ya Abdallah Sindano ambaye anakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la ubakaji na la pili ni kumwambukiza Virusi vya Ukimwi binti mwenye umri wa miaka 12 anayedaiwa kumbaka wakiwa shambani.
Mshtakiwa huyo ambaye ni mkazi wa Kata ya Goweko wilayani Uyui mkoani Tabora amepandishwa kizimbani leo, Jumanne Januari 19, katika Mahakama ya Hakimu mkazi Mkoa wa Tabora kusikiliza ushahidi wa mwisho kwa upande wa Jamhuri ambao ulitolewa na askari Polisi aliyechukua maelezo alipokamatwa baada ya kutenda makosa hayo.
Wakili Tito Mwakalinga wa upande wa Jamhuri ameieleza Mahakama ya Hakimu mkazi Tabora katika shauri hilo lililosikilizwa na Hakimu John Mdoe kwamba Jamhuri imefunga ushahidi wake ukiwa umetimiza jumla ya mashahidi wanne akiwemo daktari.
Katika kesi hiyo, mshtakiwa Sindano alimbaka binti huyo ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi huko Goweko kinyume na kifungu cha 130 na 131 sura ya 16 sheria ya mwaka 2002.
Aidha mshtakiwa huyo pia anakabiliwa na kosa jingine la kumwambukiza virusi vya UKIMWI kinyume na kifungu cha 47 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Ukimwi, Sheria namba 28 ya mwaka 2008.
Mara baada ya kusikiliza upande wa Jamhuri, Hakimu Mdoe alitoa uamuzi mdogo katika shauri hilo na kumweleza mtuhumiwa kwamba maelezo ya ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri tayari yanathibitisha anayo kesi ya kujibu na kuahirisha kesi hiyo hadi Februari 9, kesi hiyo itakaposikilizwa tena mahakamani hapo kwaajili ya utetezi.
Mshtakiwa huyo yuko nje kwa dhamana.