Siasa za Afrika | Je hotuba ya Kwanza Yoweri Kaguta Museveni Rais wa Uganda

Vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa vikisema ni “HOTUBA YA MABADILIKO YA KIMISINGI”

Kaguta Museveni akila kiapo kwa mara ya kwanza kuwa Rais wa Uganda, katika Viwanja vya bunge, Kamapala Uganda mwaka 1986

Tarehe 29 Januari 1986, Yoweri Kaguta Museveni, akiapishwa kuwa rais wa Uganda kwa mara ya kwanza, alitoa hotuba ya kusisimua kuhusu tabia za viongozi wa Afrika kung’ang’ania madaraka.

Wakati huo Museveni akiwa na umri wa miaka 39 tu, aliamsha hisia na mijadala kuhusu matatizo ya Afrika na namna yanavyohusiana na Viongozi wa Afrika kubadili katiba na kubaki madarakani.

Museveni aliwatuhumu viongozi wa Afrika wanaong’ang’ania madarakani kama kundi la watu ambao ni vibaraka wa wasioitakia mema Afrika, na kukumbatia mifumo ya wala rushwa na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Vijana wengi waliokuwa wamehudhuria mkutano wa kuapishwa kwake walivutiwa na hotuba yake. Shaka Ssali, Mwandishi mkongwe wa habari, akiwa amehitimu masomo ya Sayansi ya Siasa kutoka chuo kikuu cha Calfonia nchini Marekani, ni miongoni mwa waliohudhuria sherehe hizo za uapisho.

Katika sherehe hizo za uapisho museveni alisema, ”tatizo la Afrika siyo watu wake, bali ni Viongozi wanaong’ang’ania madarakani huku wakiwa vibaraka wa watu wasioipenda Afrika”

Vyombo mbalimbali vya Uganda na vya kimataifa viliita hotuba ya Museveni kama “A SPEECH OF FUNDAMENTAL CHANGES”

Hotuba yake ilijaa maneno ya kusisimua na kutia moyo hasa ikizingatiwa kwamba Uganda ilikuwa katika vita ya wenyewe kwa wenye.

Museveni alisema, ”yeyote anayehatarisha maisha na usalama wa waganda atakuwa ni msaliti na hapaswi kuishi kwakuwa hastahili sifa hizo”

”Yeyote anayekiuka haki za binadamu ikiwamo kuwaua raia wenzake hastahili hata chembe ya huruma, tutamdhibiti”

”Vifo vya raia wa Uganda vitokane na vifo vya asili kama uzee na magonjwa yasiyotibika, lakini siyo kutokana na mkono wa binadamu, haikubaliki”

Lakini jambo la kushangaza ni kwamba Rais Museveni wa Uganda sasa ndiye amekuwa ”role model” wa kubadilisha katiba Afrika ili kuendelea kubaki madarakani.

Kwa sasa Rais Museveni anawaita vibaraka, wote wanaompinga na yeyote ambaye anaonesha nia ya kutaka kuiongoza Uganda, huku utawala wake ukiwa umegubikwa na ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwamo utesaji, utekaji na mauaji ya raia.