Simba ‘yaachana’ na kocha wake licha ya kufuzu Klabu Bingwa Afrika

Aliyekuwa kocha wa klabu ya SImba SC  Sven Vandenbroeck

Miamba ya soka nchini Tanzania klabu ya Simba SC imetangaza kuachana na kocha wake Sven Vandenbroeck siku chache baada ya kutinga hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Barani Afrika.

Taarifa rasmi iliyotolewa na uongozi wa Simba unaelezea kuwa klabu imeachana na na kocha huyo “kwa makubaliano ya pande zote mbili.”

Hata hivyo, taarifa hiyo haikuweka wazi sababu ya kocha huyo kuondoka.

Vandenbroeck alijiunga na ‘Wekundu wa Msimbazi’ mwishoni mwa mwaka 2019, na katika kipindi cha mwaka mmoja aliohudumu katika klabu hiyo amefanikiwa kutwaa mataji matatu; Ubingwa wa Ligi, Kombe la Shirikisho pamoja na ngao ya jamii.

Licha ya mafanikio hayo, baadhi ya mashabiki na wachambuzi wamekuwa wakikosoa mbinu za kocha huyo.

Kocha msaidizi wa Simba na nahodha wa zamani wa klabu hiyo Selemani Matola kwa sasa ndiye atakayekiongoza kikosi hicho mpaka kocha mkuu mpya atakapooatikana.