AFRIKA KUSINI YAWEKA SHERIA KALI ZA KUJIKINGA DHIDI YA CORONA

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ametangaza sheria kali za kudhibiti msambao wa virusi vya corona, baada ya nchi hiyo kusajili kesi zaidi ya milioni moja ya ugonjwa wa Covid-19 kufikia sasa.

Akilihutubia taifa usiku wa kuamkia leo kwa njia ya televisheni, Rais Ramaphosa amesema serikali imepiga marufuku mikusanyiko ya aina yoyote ile ya ndani na nje ya majumba, mbali na kurejeshwa agizo la kutotoka nje kuanzia saa tatu usiku hadi 12 alfajiri.

Amesema taifa hilo lipo katika mkondo hatari wa maambukizi, haswa baada ya aina mpya ya kirusi cha corona ya Uingereza kuripotiwa nchini humo na msingi huo serikali yake imelazimika kuchukua hatua.

Rais wa Afrika Kusini ameonya watakaotembea bila barakoa katika maeneo ya umma akisisitiza kuwa, watapigwa faini au kufungwa jela kwa muda usiopungua miezi sita au yote mawili.

Amesema maagizo hayo mapya likiwemo la kufungwa maduka, mabaa na mengineo yameanza kutekelezwa saa sita usiku wa kuamkia leo Jumanne na yataendelea kuwepo hadi Januri 15.

Haya yanajiri baada ya nchi hiyo kufikisha jumla ya kesi 1,004,413 za maambukizi ya corona Jumapili ya juzi, na hivyo kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuandikisha kesi zaidi ya milioni moja ya maradhi hayo ya kuambukiza.

Inaaminika kuwa, spishi mpya ya kirusi cha corona iliyoripotiwa mara ya kwanza nchini Uingereza na inayofamika kwa kitaalamu kama 501.V2 ndiyo sababu ya ongezeko hilo la kutisha la maambukizi ya maradhi hayo nchini Afrika Kusini ndani ya siku chache zilizopita.