MKUU WA MKOA MARA AWATAKA WENYEJI KUWEKEZA MARA

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mh. Adam Malima amewataka wenyeji wa mkoa wa Mara waishio nje ya mkoa huo kurudi nyumbani na kuwekeza katika sekta mbalimbali kwani mkoa huo unazo fursa nyingi ambazo bado hazijatumika ipasavyo.

Malima amesema kuwa anasikitishwa na namba ambavyo wenyeji wa mkoa huo wameutekeleza mkoa wao licha ya kuwepo kwa vivutio pamoja na fursa nyingi za kiuchumi ambapo amewataka wenyeji hao kuungana pamoja na serikali katika kuleta maendeleo.

Amesema kuwa umefika muda sasa wana Mara kwa pamoja wanapaswa akuwa na kauli moja ya ‘Mara Yetu, Mara Moja, Fahari Yetu’ hali ambayo kwa namna moja ama nyingine itaondoa dhana iliyojengeka nchini kuwa mkoa wa Mara ni mkoa wa watu wakorofi na vitendo viovu huku akisema kuwa uwezo wa kufanya hivyo upo kinachotakiwa ni maamuzi ya wana Mara wenyewe.

Mh. Malima amesema kuwa yeye pamoja Serikali anawahitaji wenyeji hao wa Mara waishio nje ya mkoa katika kuleta maendeleo endelevu mkoani Mara huku akiahidi kutoa ushirikiano kwa wenyeji na wakazi hao kwa lengo la kuleta maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa manufaa ya mkoa wa Mara na watu wake pamoja na Taifa kwa ujumla.

Amesema kuwa fursa katika sekta za utalii, uvuvi,kilimo, mifugo, madini, elimu na nyingine nyingi zilizopo mkoani Mara zikitumika vema mkoa wa Mara utakuwa miongini mwa mikoa bora katika nyanja zote nchini na kwamba kutokana na jitihada zinazofanywa na Rais wa Tanzania Mh. Dk. John Magufuli katika kuleta maendeleo wana Mara wanatakiwa kuchangamkia fursa kwasasa kwani Rais ameonyesha mapenzi yake ya dhati kwa wana Mara hivyo wanachotakiwa kufanya ni kuunga mkono jitihada hizo kwa vitendo.

“Njooni muwekeze nyumbani fursa zipo nyingi sana, serikali yenu ipo itawapa ushirikiano sitakubali yeyote awakwamishe kwani tumechelewa sana tumechoka na sifa mbaya sasa ni muda wa kubadilisha taswra ya mkoa kijamii, kiuchumi na kimaendeleo jukumu hili ni letu sote tuliopo Mara na mliopo nje ya Mara” amesema Mh. Malima

Mwenyekiti wa kundi la WhatsApp la wenyeji wa mkoa wa Mara waishio nje lijulikanalo kama Mara Forum, Nduruma Magembe amesema kuwa wameamua kuunda umoja wao kwa lengo la kushirikiana na wana Mara pamoja na serikali katika kuleta maendeleo.