Mhe.Bashungwa tutaendelea kuyaendeleza mazuri ya Dkt. Mwakyembe

Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Innocent Bashungwa amesema kuwa mambo yote mazuri yaliyofanywa na mtangulizi wake Dkt.Harrison Mwakyembe katika sekta anazozisimamia atayaendeleza ili matarajio ya kuundwa kwa kwa Wizara hiyo yafikiwe.

Mhe.Bashungwa ameyasema hayo leo Desemba 11, 2020 wakati akipokea Ofisi kutoka kwa Waziri mstaafu Dkt.Harrison Mwakyembe ambapo ameeleza kuwa ataendelea kushauriana na naye katika masuala mbalimbali ya wizara hiyo kutokana na uzoefu aliyonao, huku akisitiza kuwa mahusiano mazuri na watu katika maeneo mbalimbali ya kazi na jamii ni muhimu kwa sababu manufaa mengi.

“Tulishirikiana na wewe katika kuhamisha Taasisi ya Haki Miliki Tanzania (COSOTA) kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara kuja wizara hii,nimatumaini yangu tutaendelea kushirikiana katika sekta zote za wizara hii”, .

Pia alisema kuwa tayari ameaviagiza Vyama vya Michezo kuwasilisha mpango mkakati wa namna ya kuendesha michezo nchini, huku akisisitiza suala la Makampuni ya Michezo ya Kubahatisha kuchangia katika ustawi wa Timu za Taifa.

Aidha,Mhe.Bashungwa ameiagiza Bodi ya Filamu Tanzania kuona namna ya kuanzisha mfumo ambao utatumika kuuza kazi za filamu kwa mfumo wa kidigitali kama ilivyo ‘Netflix’ kwani itasaidia wasanii kusambaza kazi zao kwa urahisi na pia kuchangia katika pato la taifa ambapo alisisitiza kuwa “Msanii kiwanda chake ni kichwa chake”.

Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega alisema kuwa jambo la kuwa na Shule za Michezo (Sports Academy) ni jambo la msingi ambalo uongozi wao utalifanyia kazi na kuweka mkazo katika michezo ya UMITASHUMTA na UMISETA ili timu ya taifa itokane na vijana hao.

“Tumejipanga kuhakikisha tunalinda Utamaduni wa Taifa Letu, vijana tunaowajibu wa kuhakikisha tunu za nchi pamoja na maadili ya nchi yetu tunayalinda, na katika sekta ya Sanaa tunatambua Sanaa ni ajira hivyo tutasaidia kuikuza”,alisema Mhe.Ulega.