
Mkuu wa mkoa wa Mara,Mh. Adama Malima amesema kuwa tatizo la Ukatili wa Kijinsia Mkoani Mara ni kubwa kuliko tatizo lolote mkoani hapa hivyo wadau wanapaswa kukutana kwa pamoja na kujadili Kiini, Chanzo na Ukubwa wa tatizo hilo ili kupanga kwa pamoja namna ya kulimaliza.

Akizungumza katika kongamano la kuhitimisha maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Unyanyasaji wa Kijinsia, Mh. Malima amesema kuwa jukumu la kumaliza tatizo hilo ndani ya mkoa ni la kila mtu hivyo kila mmoja anapaswa kujiuliza anatakiwa kufanya nini ili Ukatili wa Kijinsia uweze kufikia kikomo kwa malezo kuwa kila mtu ni mdau na hakuna sababu ya kukaa kimya bila kuchukua hatua.

Amesema kuwa vitendo vya Ukatili wa Kijinsia bado vinaendelea licha ya Juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali pamoja na wadau na kwamba hii ni kutokana na ukweli kuwa wahusika bado hawajaamua kuwa vitendo hivyo vikomeshwe huku akiwataka akinababa kukataa vitendo vya Ukatili kwa mabinti zao na akinamama pia kujitambua na kudai haki zao bila woga kwani serikali iko pamoja nao.
Amesema kuwa Unyanyasaji wa Kijinsia upo wa aina nyingi na kwamba chanzo chake kinaanzia kwenye familia na kuzitaka mamlaka zinazohusika ikiwepo Dawati la Polisi la Jinsia kubadilisha utendaji wao wa kazi kutokana na madai ya kushindwa kutoa msaada kwa waathirika wa vitendo hivyo pale wanapowafikia kwa msaada zaidi.
You must be logged in to post a comment.