
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameliahidi Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Watoto duniani (UNICEF) kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itaendeleza ushirikiano na Shirika hilo ili kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi.
Rais Dk. Hussein aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alikutana na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Watoto duniani (UNICEF) nchini Tanzania Bi Shalini Bahuguna ambapo mbali ya mazungumzo hayo Mwakilishi huyo alifika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha.
Rais Dk. Hussein Mwinyi alitumia fursa hiyo kwa kulipongeza na kulishukuru Shirika la UNICEF kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha malengo ya Shirika hilo yanafikiwa hapa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuimarisha ustawi wa watoto kwa kusaidia huduma mbali mbali zikiwemo zile za kijamii.
Rais Dk. Hussein alisema kwamba Serikali ya Awamu ya Nane iko tayari kushirikiana na Shirika hilo katika maeneo ya kipaumbele yaliyowekwa katika kuhakikisha mafanikio yanafikiwa.
Aidha, Rais Dk. Hussein alitumia fursa hiyo kulipongeza Shirika hilo kwa kuendelea kusaidia uimarishaji wa huduma za kijamii hapa Zanzibar hatua ambayo imekuwa ikiwasaidia watoto, vijana na hata wanawake.
You must be logged in to post a comment.