
Katumba ni mgombea binafsi wa nafasi ya urais, pamoja na Henry Tumukunde Kakurugu, na Nancy Linda Kalembe. Kura za maoni zimempendelea kijana huyo ambaye alipata asilimia 70 za ushindi, huku Museveni akipata asilimia 15, na Robert Kyagulanyi akiambulia asilimia 17. Umri wake umekuwa na gumzo ambapo duru za kisiasa zimebainisha kuwa ni ishara ya mafanikio ya demokrasia.
Inaelezwa kuwa kulingana na umri wake, harakati za siasa jinsi zilivyo zinamfanya kuwa miongoni mwa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa siku zijazo pamoja na kugombaniwa na vyama vya kisiasa.
Aidha, vijana katika ukanda wa Afrika mashariki wamepewa ujumbe kwa hatua ya John Katumba kuwa na ari, matumaini, uthubutu na dhamira halisi ya kuwatumikia wananchi na kutuma ujumbe kuwa kikwazo cha umri wa wagombea hakiwezi kuwa na manufaa tena na kwamba hizi ni zama za mabadiliko ya uongozi kwenda kwa kizazi kipya.

Katumba anawakilisha kizazi kilichosoma historia ya hekaheka za Museveni kushika madaraka zilizoanzia nchini Tanzania, ambako amewahi kushiriki mkutano maarufu unaojulikana kama Kongamano la Moshi ‘The Moshi Conference’ wa wapigania ukombozi wa nchi hiyo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro kaskazini mwa Tanzania.
Aidha, duru za usalama nchini zinaeleza kuwa Museveni alinusurika kukamatwa na wanausalama wa uliokuwa utawala wa Iddi Amin katika kipindi ambacho alikuwa kiongozi wa kikundi cha Fronasa na baadaye NRM.
Wakati huo aliungana na wapigania ukombozi wengine kama vile ‘Kikosi Maalumu” cha Milton Obote, Tito Okello, Yusufu Lule (UNFL), David Oyite Ojok, Akena p’Ojok(SUM), William Omaria na Ateker Ejalu, Godfrey Binaisa, Andrew Kayiira na Olara Otunnu wa kikosi cha UFU.
Na sasa vijana wameamua kuweka wazi kuhitaji mamlaka ya kuendeleza mustakabali wao na kutuma ujumbe kwa kiongozi huyo mkongwe kuwa zama zake za kujivunia historia hii huenda zikafika tamati na si kigezo tena cha kusalia mamlakani.
Ikumbukwe Yoweri Tibabuhurwa Kaguta Museveni alipochukua madaraka kuongoza Uganda mwaka 1986 alikuwa kijana wa miaka 42. Miaka 34 baadaye anaingia kwenye kinyang’anyiro cha kutetea kiti chake dhidi ya ‘mjukuu wake’ wake John Katumba, ambaye wakati anazaliwa rais huyo mkongwe kuliko wote Afrika mashariki alikuwa ametimiza miaka 28 madarakani.
You must be logged in to post a comment.