TANZANIA HAJAWEKEWA VIKWAZO NA UMOJA WA ULAYA

Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na EU Jestus Nyamanga amekanusha vikali juu ya ripoti za kupitishwa kwa azimio la Bunge la EU dhidi ya Tanzania.

“Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Umoja wa Ulaya ilikutana Novemba 19, 2020 katika kikao chake cha kawaida, moja ya mada zilizozungumziwa ni Tanzania na hali ilivyo baada ya uchaguzi mkuu kukamilika.

Huu ni utaratibu wa kawaida wa Kamati ya Bunge la Umoja wa Ulaya kujadili kuhusu nchi ambayo ni mbia wao wa maendeleo pindi tu uchaguzi unapokamilika katika nchi hiyo na hasa uchaguzi mkuu.

“Kuna taarifa zinaenezwa katika mitandao ya jamii, ni taarifa za upotoshaji na zisizo na ukweli wowote zikidai eti Bunge lote la Umoja wa Ulaya limeazimia kusitisha misaada na mikopo kwa Tanzania pamoja na mashirika yake.

Pia taarifa hizo pia zinadai eti Bunge la Umoja a Ulaya limeiwekea Tanzania vikwazo pamoja na kuzuia kuuza bidhaa zake kwa jumuiya hiyo. Taarifa hizi ni za uongo mtupu na zenye lengo la kupotosha.

“Kikao cha Bunge la Umoja wa Ulaya kilichokaa Novemba 19, 2020 ni cha Kamati ya Mambo ya Nje ya bunge hilo na sio kikao cha bunge lote la Umoja wa Ulaya.

Lakini pia hata kikao hicho hakikutoa azimio lolote kuhusu Tanzania. Kilichofanyika katika kikao cha Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Umoja wa Ulaya ni kuwapa wajumbe nafasi ya kutoa mawazo yao binafsi kuhusu hali ya Tanzania baada ya uchaguzi na ni wabunge watano tu waliotoa mawazo yao kati ya wabunge 71 wa kamati hiyo.

“Bunge lote la Umoja wa Ulaya lina jumla ya wabunge 705, waliozungumza katika kamati ni wajumbe watano tu na walitoa mawazo yao kwa jinsi wanavyoona, siyo azimio wala makubaliano yaliyowekwa.

Taarifa hizo zinaenezwa na watu wenye nia mbaya na Tanzania, taarifa pia zinadai kuwa Bunge la Umoja Umoja wa Ulaya limeazimia kuifutia Tanzania msaada wa euro milioni 626 ambazo hupewa na umoja wa Ulaya, si kweli fedha hizo hupewa Tanzania kila mwaka.

“Utekelezaji wa miradi ya Umoja wa Ulaya unaendelea vizuri na hakuna azimio lolote la kusitisha fedha kutoka Jumuiya hiyo na wapotoshaji hao wanadai eti kuna majadiliano yanaendelea ya kuiwekea vikwazo vya kiuchumi Tanzania, hakuna majadiliano hayo.

Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Umoja wa Ulaya kama ilivyo kwa kamati za Bunge la Tanzania, wabunge wake wana uhuru na kutoa mawazo yao katika majadiliano mbalimbali na mawazo yao hayawi azimio hadi tu pale itakapoamriwa na Bunge lote.

“Nawaomba niwahakikishie Watanzania wenzangu, Uhusiano wa Tanzania na Umoja wa Ulaya ni mzuri tena mzuri sana, kwa zaidi ya miaka 45 tangu 1975, kwa kipindi chote hicho tumekuwa na uhusiano mzuri na kuendelea kushirikiana,” amesema Balozi Jestas Nyamanga.

“Umoja wa Ulaya haujasitisha misaada ya mikopo Tanzania”

Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na EU Jestus Nyamanga