
Maadhimisho hayo ya mwaka huu yalipewa kauli mbiu isemayo ‘Wekeza katika kukinga na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza, Onyesha kwa Vitendo’
Dar es Salaam: Takwimu za Kitaifa juu ya hali ya magonjwa yasiyoambukiza zinaonesha tatizo hilo lipo nchini na linaongezeka kwa kasi, ongezeko likiwa asilimia 24 ndani ya miaka miwili.

Akizungumza wakati wa kufunga maadhimisho ya wiki ya Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza mapema leo kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge amesema hilo ni ongezeko kubwa na linahitaji mikakati madhubuti ili kukabiliana nalo.
“Magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa tishio siyo tu kwenye jamii yetu bali ulimwenguni kote, takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha mwaka 2018 yalichangia zaidi ya vifo milioni 41, hii ni sawa na asilimia 71 ya vifo vyote milioni 57 vilivyotokea mwaka 2018,” amebainisha Rc. Kunenge.
Amesema taarifa za mwaka 2013 za Shirika la Maendeleo Duniani (UNDP) zinaonesha kwamba pamoja na changamoto hizo za kiafya, magonjwa hayo pia yanaathiri Nyanja nyingine za maisha na jamii kwa ujumla.
“Inakadiriwa ifikapo 2033 gharama zitokanazo na huduma kwa magonjwa haya zitafikia Dola za Marekani trilioni 47, fedha ambazo zingeweza kutumika kupunguza umaskini kwa watu bilioni 2.5 kwa miaka 50.
“Kwa nchi zenye uchumi wa kati na chini, magonjwa haya yatagharimu mataifa hayo jumla ya Dola za Marekani trilioni saba kwenye kipindi cha 2011 hadi 2025,” amesema.
Rc. Kunenge ameongeza “Gharama hizi zinatokana na huduma za matibabu na nguvu kazi inayopotea ‘loss productivity’ kutokana na maradhi hayo.
Amesema makadirio yanaonesha gharama za huduma za magonjwa hayo itafikia asilimia 75 ya mzigo wa bajeti duniani huku ugonjwa wa kisukari ukipelekea gharama zaidi ya Dola za Marekani bilioni 465 sawa na asilimia 11 ya bajeti yote ya afya duniani.
“Ni muhimu kujikinga dhidi ya magonjwa haya, kwa sababu ni gharama kuyatibu, kwa mfano wagonjwa wenye matatizo ya figo kushindwa kufanya kazi huhitaji kupatiwa huduma ya kusafisha damu angalau mara tatu kwa wiki.
“Gharama za kusafisha damu kwa kwiango cha kawaida katika hospitali za Serikali ni Sh. 200,000 kwa siku.
“Bila ya kuweka gharama nyingine za matibabu, usafiri na chakula, katika wiki moja mgonjwa mmoja anahitaji angalau Sh. 600,000, kwa mwezi atatumia Sh. milioni mbili hadi nne ambayo ni sawa na wastani wa Sh. milioni 28 kwa mwaka.
“Gharama hizi ni kubwa kwa watanzania hivyo nafuu ya magonjwa haya ni kuzuia tusipate, inatupasa kuunganisha nguvu pamoja katika kuzuia vihatarishi, kuhamasisha jamii kushiriki kwenye mazoezi au shughuli za nguvu, kuzingatia mlo unaofaa hasa kuondoa au kupunguza chumvi, sukari na mafuta,” amesisitiza.
Awali, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Grace Maghembe amesema katika kuadhimisha wiki hiyo jumla ya vipindi 30 vimefanyika kuelimisha wananchi.
“Tumeweza kuwafikia wanafunzi 1,000 katika shule 50 zikiwamo za msingi na sekondari na kuwapa elimu, tumetoa matangazo zaidi ya 40, tumepokea machapisho ya tafiti 200 zilizofanyika nchini katika kongamano la kisayansi la magonjwa yasiyoambukiza ambalo lilihudhuriwa na washiriki zaidi ya 500,” amesema.
Ameongeza “Zaidi ya watumishi na wana vikundi vya jogging wameshiriki matembezi mbalimbali, kulikuwa na michezo mbalimbali.
“Katika huduma za upimaji hapa Mnazi Mmoja wananchi 1,012 walionwa Novemba 12, 3,867 walionwa Novemba 13, katika siku hizi mbili tuliona jumla ya watu 4,879 na kuwahudumia,” amebainisha.
Amesema wananchi wamechunguzwa macho, moyo, masikio, saratani, ngozi shinikizo la damu na kupatiwa huduma za ushauri wa lishe na bima ya afya.
Mwenyekiti wa Chama cha Wagonjwa wenye Kisukari, Prof. Andrew Swai ameshauri jamii kurudi katika asili akitoa mfano kula vyakula visivyokobolewa ili kuepuka magonjwa hayo.
“Kwa sababu kasi ya magonjwa haya inaongezeka, utafiti wa mwaka 1980 unaonesha kulikuwa na mgonjwa mmoja kati ya watu 100 wa kisukari siku hizi katika kila watu 100 kuna wagonjwa 26, tulikuwa na wodi moja ya saratani sasa tuna jingo zima na wagonjwa wanajaa,” ametoa mfano.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO- Tanzania), Dk. Galbert Fedjo ameipongeza Tanzania kwa jitihada kubwa zinazofanyika katika kukabiliana na kasi ya magonjwa hayo.
Amesema WHO lipo tayari kushirikiana bega kwa began a Serikali katika kuongeza nguvu ya mapambano hayo.
“Tanzania imeanza utekelezaji kufikia malengo Endelevu ya Dunia (SDGs) hasa namba tatu linalosisitiza kuhusu afya bora na kipekee kipengele cha 3: 4 ambacho kinagusa moja kwa moja magonjwa yasiyoambukiza.
“WHO tunatoa ushirikiano kwa Tanzania katika kuboresha huduma katika ngazi ya vituo kwa mfano upatikanaji wa dawa za kisukari, tutaendelea kutoa ushirikiano wetu,” amesisitiza.
You must be logged in to post a comment.